JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA

Kamandi ya Jeshi la Kujenga Taifa

UTANGULIZI

  • Moja ya vyombo vilivyoundwa na Serikali ya Tanganyika mara tu baada ya Taifa hili kupata uhuru ni Jeshi la Kujenga Taifa lililoasisiwa tarehe 10 Jul 1963.  Jeshi la Kujenga Taifa kwa kifupi JKT, liliundwa ili kuponya majeraha yaliyoachwa na serikali ya kikoloni miongoni mwa jamii ya watanzania ambayo ni pamoja na
    ubaguzi wa kidini, makabila, rangi na kipato. Chombo hiki ni muhimu katika kuelimisha na kuandaa vijana wa kitanzania kiuzalendo, kimaadili, kinidhamu na kuwafanya wawe raia wema wanaopenda kutumikia na kulinda nchi yao.  
  • Vikosi vya JKT ni mahali ambapo vijana hupata fursa ya kujifunza kwa vitendo, maana na umuhimu wa kazi pamoja na kutoa huduma kwa Taifa lao bila kutegemea kulipwa ujira wowote. Imedhihirika wazi kuwa wajibu wa JKT katika maendeleo ya Taifa hili ni mkubwa na muhimu sana.  Nchi mbalimbali duniani zina taasisi zinazofanana na taasisi yetu ya JKT. Kwa msingi huo nchi yetu kuwa na JKT ni jambo la kujivunia, yvilevile ni chombo cha kujenga Umoja na Utaifa kwa vijana wetu, kwa ufupi JKT ni jando la vijana kitaifa kwa watanzania.

HISTORIA YA JKT

Kuanzishwa kwa JKT, kulitokana na mawazo ya Umoja wa Vijana wa Chama cha TANU (TANU Youth
League). Katika Mkutano wao Mkuu uliofanyika mjini Tabora tarehe 25 Aug 62, chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja huo, hayati Joseph Nyerere.  
  
Tarehe 19 Apr 63, Baraza la Mawaziri la Tanganyika chini ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika
na Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere, lilipitisha Azimio la umoja wa vijana wa TANU na kuamua kwa kauli moja kuazishwa JKT mnamo tarehe 10 Jul 1963.  Kundi la kwanza lilipata mafunzo katika kambi ya Mgulani Dar es salaam likiwa na jumla ya vijana 11 toka wilaya 11 tofauti.

SHERIA YA KUANZISHWA KWA JESHI LA KUJENGA TAIFA NA MAREKEBISHO YAKE

Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa kwa sheria ya ‘Nationa Service Act No 16’ ya mwaka 1964.  Sheria hii inatoa uwezo wa Jeshi la Kujenga Taifa kuandikisha vijana wa kulitumikia taifa.  Aidha, sheria hii imeendelea kufanyiwa marekebisho kutokana na mahitajio, baadhi ya marekebisho hayo ni:-

a.     Marekebisho ya mwaka 1966

Tangu lilipoasisiwa JKT lilikuwa linaandikisha vijana wa kujitolea wenye elimu ya chini tu.  Ilipofika mwaka 1966, ilionekana kuwa, kuna umuhimu wa vijana wasomi wenye elimu zaidi ya kidato cha nne kulitumikia JKT.  Hivyo, sheria ilirekebishwa ili kulipa JKT nguvu za kisheria ili liweze kuandikisha vijana wenye taaluma zaidi ya kidato cha nne kwa mujibu wa sheria (Compulsory service).

b.     Marekebisho mengine ni ya mwaka 1975 wakati JKT lilipounganishwa rasmi na JWTZ, hivyo kulifanya JKT kuwa moja ya Kamandi zilizo chini ya JWTZ. Sambamba na marekebisho hayo, shughuli za JKT ziliwekwa bayana kuwa ni:-

       (1)    Kuwafundisha vijana wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulitumikia Taifa katika nyanja za      

        kijamii, maendeleo ya uchumi na ulinzi wa Taifa.

       (2)    Kutoa mafunzo ya msingi ya Jeshi kwa vijana kwa lengo la kuwawezesha vijana hao kufikia sifa     

        ya   kujiunga katika vyombo vya Ulinzi na Usalama kama JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa na Magereza.

      (3)    Kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa Taifa.

c.     JKT katika shughuli za malezi ya vijana lilijihusisha na uzalishaji mali, shughuli hii ilipata nguvu zaidi mwaka 1981 pale ambapo Shirika la Uzalishaji Mali au kwa kifupi SUMAJKT lilianzishwa kisheria kupitia
‘The Corporation Sole Establishment Act of 1974’. Lengo la kuanzisha SUMAJKT ni kusaidia miradi ambayo ilikuwa na uwezo mkubwa wa uzalishaji iweze kuzalisha zaidi. Faida itakayopatikana isaidie serikali katika kupunguza matumizi katika kuendesha shughuli za JKT.

DIRA, DHIMA, MAJUKUMU NA MAADILI YA MSINGI

   a.     Dira

    Kupitia JKT, Tanzania iwe ni nchi ambayo vijana wake watalelewa vizuri katika malezi yaliyo bora wakiwa     

     wenye:-

    (1).     Nidhamu

    (2).     Kujiamini

    (3).     Moyo wa uzalendo na kuipenda nchi yao

    (4).     Umoja na Udugu

    (5).     Moyo wa kupenda kazi

    (6).     Kutekeleza wajibu wao.

Vijana hao wa mwanzo walikuwa makatibu wa umoja wa vijana ambao mwaka 1962 walipelekwa na TANU
nchini Yugoslavia, kujifunza mafunzo ya uongozi wa vijana. Baadhi ya vijana hao watangulizi ni Bi. Z. Kiango, Bw. S. Chale, Bw. P. Lwegarulira, Bw. R. Kamba, Bw. H. Ngalason, Bw, J.Ndimugwango, Bw. S. Desai, Bw. D. S. Msilu (Master), Mr ES Mwakyambiki, (Senior Master) na Mr AI Msonge (Master), Mr LM Mitande.

   b.     Dhima
Kuwalea vijana wa Tanzania ili wawe na nidhamu, uzalendo na ujuzi ambao utawawezesha kushiriki kikamilifu
katika Ulinzi, Usalama pamoja na Ujenzi wa Taifa.

Majukumu ya JKT

(1)   Malezi ya Vijana:- 

       (a).    Vijana kufundishwa moyo wa kupendana bila kujali tofauti za itikadi, dini,
        kabila, kipato na jinsia.

       (b).    Kupenda kazi za mikono.

       (c)    Kuthamini na kuendeleza mila, desturi na kudumisha utamaduni wa Taifa. 

       (d)    Kuwa raia wema, wanaojiamini, wanaojituma, wenye uzalendo na kuipenda nchi yao. 

(2)    Ulinzi wa Taifa

        (a)    Kuwapa vijana mbinu za kijeshi ili wawe Jeshi la akiba, kuwaandaa vijana watakaofaa kujiunga   

         na     vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.

         (b)    Kuwaandaa vijana kusaidia katika majanga mbalimbali, mfano mafuriko, moto na ajali mbali mbali.

(3)   Uzalishaji Mali

Ili kuwafanya vijana wa kitanzania waepukane na kusumba kuwa kazi za ofisini ndio njia pekee na bora
inayomuwezesha mtu kuishi. JKT linafundisha ufundi, stadi za maisha na ujasiliamali kuwawezesha vijana kujiajiri katika sekta mbali mbali mara baada ya kumaliza mikataba wao JKT.  Uzalishaji mali unaofanywa na JKT ni pamoja na:-

      (a)  Kilimo na ufugaji.

      (b)  Fundi uashi, seremala,umeme na makanika.

      (c)  Ushonaji.

Maadili ya msingi  

JKT linaendeshwa kwa kufuata misingi na maadili ya kujenga umoja na mshikamano wa Kitaifa. Maadili ya msingi ya JKT ni yafuatayo:-

(1)    Uadilifu.  JKT huwajenga vijana kuwa waaminifu, wakweli na wa kutegemewa na Taifa.

(2)    Kujitolea.  Kuandaa vijana kuwa na moyo wa kujituma na kujitolea.

(3)    Umoja na Mshikamano.  Kuandaa vijana kuwa jamii yenye mshikamano na umoja wa kitaifa bila kujali itikadi zao za kitamaduni, kisiasa na kidini.

(4)    Uzalendo. JKT huwaandaa vijana wawe na moyo wa uzalendo, udugu na kuipenda nchi yao.

(5)    Nidhamu. Kuwafundisha vijana kuwa watiifu na wenye heshima.

(6)    Kupenda kazi.  Kuwaanda vijana kuwa jamii yenye kutekeleza wajibu na moyo wa kupenda kufanya kazi.

MAFANIKIO YA JKT KWA UJUMLA

Kwa ujumla JKT limefanikiwa katika nyanja mbali mbali kama ifuatavyo:-

a.     JKT limesaidia sana uimarishaji umoja wa Kitaifa.

b.     Vijana wengi waliopitia JKT wameonesha moyo wa kupenda kazi za mikono, kujituma na
kujiheshimu.

c.     Miongoni mwa vijana waliopitia JKT wameonesha kuwa viongozi mahiri, wachapa kazi, wenye nidhamu, wabunifu na wavumilivu.

d.     Vijana wa JKT wamechangia kwa kiasi kikubwa katika kuthamini na kuhifadhi  utamaduni wa Taifa.

e.     JKT limetoa wanamichezo bora, wenye viwango vya Kitaifa na Kimataifa na hivyo kuliletea sifa  Taifa letu.

f.      JKT ni asasi ya aina yake hapa nchini iliyowaweka vijana wake tayari kutumikia nchi katika mazingira ya aina mbalimbali kwa mfano, wakati yanapotokea majanga ya mafuriko, moto, ajali nyinginezo na vita.

g.      JKT ni chuo cha ufundi, kilimo na stadi za kazi mbalimbali ambapo maelfu ya vijana waliopitia JKT wanaendesha maisha yao kwa kutumia ujuzi na uzoefu walioupata JKT.

h.     JKT limekuwa mfano wa kuigwa na mataifa jirani na hivyo kupelekea mataifa hayo kuanzisha shughuli za malezi ya vijana katika nchi zao mfano JKU Zanzíbar, Zambia na Guyana.

j.      JKT kupanuka kitaaluma ambapo kupitia SUMA JKT, wataalam wake hutumika katika shughuli za ushauri ‘Consultancy’.

i.      Hifadhi wa mazingira umepewa umuhimu mkubwa ambapo  asasi na wananchi wanaoishi jirani na vikosi/makambi ya JKT hupewa miche ya miti bure au huuziwa kwa bei ya chini ili kuwawezesha kutunza na kuhifadhi mazingira

 Malezi ya Vijana
liliendelea kutoa mafunzo ya malezi kwa vijana wa kujitolea na mujibu wa sheria na matunda yake yalidhihirika katika maeneo mengi mfano, miaka ya 1983 - 84, vijana wa JKT kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walishiriki kikamilifu katika kuwasaka na kuwakamata wahujumu uchumi na Ops Linda Jiji. Operesheni zilizoendeshwa kwa wakati huo ni :-

       (a)     UJENZI  1980

       (b)    TIJA    1980

       (c)     JUHUDI 1981

       (d)     IMARISHA 1981

       (e)    TEKELEZA “B” 1982

       (f)     KUJIHAMI   1982

       (g)     SAFISHA   1983

       (h)     NGUVU KAZI   1983

       (j)      MSHIKAMANO  1984

       (k)     WAJIBU   1984

       (l)      VIJANA  1985

      (m)     OKOA  1985

      (n)      AWAMU YA PILI   1986

      (o)      NIDHAMU   1986

      (p)      CCM MIAKA 10  1987

      (q)      MIAKA 20 YA AZIMIO LA ARUSHA 1987

      (r)      KIZOTA  1988

      (s)      MIAKA 25 YA JKT  1988

      (t)       MPITO  1989

      (u)      PROGRAM YA CHAMA 1989